htAflog

MPYA: TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

          

TUNAKANUSHA KWA NGUVU ZOTE UPOTOSHAJI WA MAKUSUDI WA GAZETI LA ‘HABARI LEO’ KUHUSU HIZB -UT TAHRIR

Gazeti la ‘Habari Leo’ la tarehe 26/10/2012 katika ukurasa wa nne, katika kuripoti matukio ya vurugu la Zanzibar na waliokamatwa baada ya vurugu hizo liliripoti uzushi, upotoshaji wa makusudi, uwongo wa wazi, na  kwa hakika  wa kushangaza kamwe kuhusu Chama cha Kiislamu cha Kilimwengu cha Hizb-ut Tahrir

Gazeti hilo la ‘Habari leo’ la tarehe tulioitaja hapo juu liliandika haya yafuatayo

 

“Wakati kukiwa na habari zinazomuhusu sheikh Farid, Ziko pia taarifa kwamba miongoni mwa wanaotuhumiwa sambamba  na yeye kuna mmoja anaedaiwa kuwa mwakilishi wa kikundi cha Kiislamu cha Boko Haram cha Nigeria akiwakilisha katika Afrika Mashariki kutokea Mombasa Kenya. Nchini wafuasi wake wanadaiwa kutumia jina la Hizb-ut Tahrir, na alipata kutambulishwa katika viwanja vya Magomeni takriban miaka miwili, wamekuwa na mkakati wa kuchoma makanisa na baa” [Chanzo http://habarileo.co.tz/index.php/habari-za-kitaifa/5392-shekhe-farid-achunguzwa-kuhusu-al-qaeda]

Kwa taarifa hii gazeti la ‘Habari Leo’ kwa makusudi limeleta uzushi na upotoshaji wa makusudi kwa  kukusudia kuonyesha baadhi ya uwongo ufuatao

1. Kwamba Mashababu/vijana wa Hizb-ut Tahrir wanashiriki katika mchakato wa wimbi la harakati za kizalendo/Aswabia za kupigania uzanzibari zilizovishwa guo la kidini. Kitu ambacho si kweli, kwa kuwa Hizb ut Tahrir inajifunga na hukmu za Kiislamu pekee ambazo zimeweka wazi uharamu wa kulingania fikra za utaifa na uzalendo/Aswabia. Na isitoshe Uislamu umeweka wazi njia ya kuitumia kuondoa dhulma zote na sio kupitia njia ya haramu

2> Kwamba katika watuhumiwa waliokamatwa katika ..vurugu la Zanzibar miongoni mwao ni kutoka Chama cha Hizb- ut Tahrir, ilhali wawakilishi rasmi kwa vyombo vya habari wa Hizb ut -Tahrir Afrika Mashariki hawajatoa uthibitisho huo

3. Kuchochea fikra hatari na ya upotoshaji kwamba Hizb-ut Tahrir ni tawi la Boko Haram la Nigeria. Tuhuma hizi ni za uwongo wa wazi na hazina msingi wowote. Hakuna uhusiano kwa namna yoyote baina Hizb-ut Tahrir na Boko Haram. Hizb-ut Tahrir ni chama cha Kiislamu cha kilimwengu tangu mwaka 1953. Njia yake ya mageuzi inaeleweka na kila mtu tangu kuundwa kwake kwamba ni njia aliyoitumia Mtume SAAW ambayo haihusishi utumiaji wa vitendo vya nguvu, vurugu wala mabavu. Licha ya kuwa wanachama na wafuasi wake wakati mwengine hutendewa vitendo vya dhulma na ukandamizaji hususan na serikali za kidikteta.

4. Kwamba, Kongamano lililofanywa na Hizb-ut Tahrir Afrika Mashariki miaka michache iliyopita hapo Msikiti wa Kichangani, Magomeni, Dar es- Salaam lilitambulisha viongozi wake na mafungamano yake na Boko Haram. Jambo hili ni uwongo wa wazi. Kauli kama hii ya ‘Habari Leo’ ndio kauli ya mwanzo kutolewa katika maelfu ya waliohudhuria Kongamano hilo vikiwemo vyombo mbalimbali vya habari

Baada ya hayo, tunasema upotofu huu wa ‘Habari Leo’ ni wa makusudi uliodhamiria kuipaka matope Hizb- ut Tahrir, kuharibu haiba yake njema mbele ya umma, kuwatisha wasiokuwa Waislamu kwa kuwatia khofu juu ya Uislamu. Aidha, inajihidhirisha waziwazi zaidi namna gazeti la ‘Habari leo’ lilivyodhamiria kucheza karata hatari ya ‘udini’ ndani ya Tanzania na kuwa kifua mbele katika uadui wa kilimwengu dhidi ya Uislamu, Waislamu na Taasisi zao. Tunasisitiza tena upotoshaji huu ni wa makusudi kwa sababu mbili kubwa:

Kwanza, gazeti la ‘Habari Leo’ ni miongoni mwa vyombo vya habari vilivyoripoti na kuangazia Kongamano letu tulilolifanya hapo Msikiti wa Kichangani, Magomeni miaka michache iliyoipita, na kamwe kwa kipindi chote halikuwahi kutaja tuhuma hizo za uwongo inazozitaja leo. Isitoshe ndani ya Kongamano hilo Hizb -ut Tahrir Ukanda wa Afrika Mashariki ilichawanya vipeperushi kwa maelfu, ilifanya mkutano na waandishi wa habari na kuongeza kueneza maandishi mbalimbali hata baada ya Kongamano kufafanua kwa upana historia, malengo na njia ya Hizb-ut Tahrir katika kuleta mageuzi. Na katika hayo yote hakukutajwa chochote kuhusu fungamano la Hizb na Boko Haram, si uvu makanisa wala utumiaji wa nguvu na mabavu katika kufikia malengo ya Hizb ut Tahrir. Sasa leo hii, taarifa hizi gazeti la ‘Habari Leo’ imezipata wapi

Pili, Hizb-ut Tahrir ina Wawakilishi wake rasmi kwa Vyombo vya Habari ambao ndio dhamana wa kutoa kauli, maelezo na ufafanuzi kuhusiana na jambo lolote la Hizb. Na kimsingi baadhi hata ya waandishi\maripota wa gazeti la ‘Habari Leo’ wanawajua binafsi wanachama wa Hizb Ut Tahrir. Basi iweje Habari Leo kuruka mipaka kuandika uwongo kama huu bila ya kupata ufafanuzi kutoka kwetu kama si kuwa na nia mbaya

Msimamo wetu

Tunayakanusha yote yaliyosemwa na gazeti la ‘Habari Leo’ la tarehe tuliyoitaja. Na tunalitaka (demand) gazeti hilo kuomba radhi rasmi na kurekebisha katika kipindi cha wiki moja uwongo waliouandika katika gazeti lao kwa makusudi kuanzia tarehe ya taarifa hii

Na zaidi, tunatoa mwito kwa gazeti hilo na vyombo vyengine vya habari vishikamane na maadili ya uandishi wa habari na sio kujiingiza katika fedheha kama ya gazeti hili

Kushindwa gazeti la ‘Habari Leo’ kuchukua hatua tulizozitaja, tunalieleza gazeti hilo, kwa uwongo waliozua kamwe hawatoudhuru Uislamu wala Hizb-ut Tahrir, bali litajidhuru nafsi yake. Kwa kuwa vitendo viovu havimzingiri ila anayevitenda.

..‘Na vitendo viovu havimzunguuki ila aliyevifanya…. (TMQ
35:43)

                                                            

Masoud Msellem

Naibu Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari

Afrika Mashariki

Comments are closed.